Real Madrid tayari wako nje ya mashindano ya Kombe la Mfalme baada ya kupokea kipigo cha 2-1 kutoka kwa Leganes ndani ya uwanja wao wa nyumbani, Bernabeu jana Jumatano. Ni Javier Eraso na Gabriel Pires waliofunga mabao ya Leganes huku Karim Benzema akifunga la Rea ambao wameondolewa kwa sheria ya bao la ugenini baada ya kuwa walishinda mchezo wa kwanza kwa 1-0 huko Estadio Butarque wiki iliyopita.
Hiki ni kipigo cha nne ndani ya uwanja wao wa nyumbani msimu huu wakiwa wamepoteza pia michezo mitatu ya La Liga kwenye uwanja huo dhidi ya Real Betis Septemba mwaka jana, dhidi ya Barcelona Disemba mwaka jana na dhidi ya Villarreal wiki mbili zilizopita. Girona na Tottenham Hotspur wanaongeza orodha ya wababe wa vijana hawa wa Zidane msimu huu ambapo timu hizo mbili zilipata ushindi kwenye viwanja vyao vya nyumbani.
Kuwa nyuma ya vinara FC Barcelona kwa alama 19 kwenye mashindano ya La Liga kunaleta picha kuwa Zidane anahitaji miujiza kuwapiku mahasimu wao hao na kutwaa taji hilo. Kuondolewa na Leganes kwenye hatua ya robo fainali ya Kombe la Mfalme kunamuweka mahala pabaya zaidi kiungo huyu wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa licha ya mafanikio makubwa aliyoipatia klabu hiyo kwenye misimu miwili iliyopita.Nini hatma ya Zinedine Zidane kuhusu kibarua chake? Jumamosi anakwenda kuwatembelea Valencia ndani ya dimba la Mestalla kwenye mchezo wa La Liga. Valencia walio mbele ya Real Madrid kwa alama tano wakiwa kwenye nafasi ya tatu wanaweza kuwapa wakati mgumu mno Real Madrid walio kwenye nafasi ya nne. Zidane anatakiwa kushinda mchezo huu kwani matokeo mabaya yatamuweka kwenye wakati mgumu zaidi.
Mfaransa huyo anahitaji ushindi kwenye mchezo huo wa Jumamosi na kisha matokeo mazuri kwenye michezo wa La Liga unaofuata dhidi ya Levante ugenini na kisha dhidi ya Real Sociedad wa nyumbani Santiago Bernabeu ili arejeshe kiasi fulani cha imani juu ya uwezo wake wa kuendelea kukinoa kikosi cha matajiri hao kutoka jiji la Madrid.
Hata hivyo kuna kafara muhimu zaidi anayotakiwa kutoa Zinedine Zidane ili ajihakikishie usalama wa kusalia kama mwalimu wa klabu hiyo yenye rekodi ya kuwa na uvumilivu kiduchu mno na mameneja hata waliowapa kiasi fulani cha heshima na mafanikio. Mwalimu Carlo Ancelotti anaweza kulisimulia hili vizuri zaidi.
Zidane anahitaji kuwatoa kafara matajiri wa Ufaransa, PSG mwezi ujao kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa, ili kulinda kibarua chake. Hili hata hivyo, haliwezi kuwa rahisi hata kidogo. Ngome ya Real Madrid inaonekana kuwa dhaifu mno wakati PSG wapo kwenye kiwango kizuri mno msimu huu waking’arishwa na kiwango safi cha Neymar aliyejiunga nao Agosti mwaka jana.
PSG wanaoongoza jedwali la Ligi Kuu ya Ufaransa kwa tofauti ya alama 8 dhidi ya Lyon walio kwenye nafasi ya pili ni moja kati ya timu tishio mno kwa sasa barani Ulaya. Ni timu pekee yenye uwiano mkubwa wa magoli kwa kila mchezo kuliko timu yoyote kwenye ligi tano kubwa za barani Ulaya ikiwa na uwiano wa mabao 3.1 kwa mchezo. Zidane ana kibarua kizito cha kufanikisha kafara yake hii muhimu.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya pia wameonesha moto wa hali ya juu wakiwa ndio timu yenye mabao mengi zaidi msimu huu. Wamefunga mabao 25 kwenye hatua ya makundi idadi ambayo ni ziadi ya mara mbili ya idadi ya mabao ya klabu tishio kama FC Barcelona kwenye michuano hiyo ya Ulaya.
Zidane mwenyewe amekiri kuwa kibarua chake kitakuwa kwenye hatari kubwa mno ikiwa atashindwa kuwaondoa PSG kwenye hatua ya 16 Bora. Yuko sahihi mno kwenye hili. Anahitaji kunusuru kibarua chake kwa kuwatoa kafara ya Neymar na wenzie. Lakini atambue wazi kuwa kafara hii muhimu ni ngumu mno kuifanikisha.
No comments:
Post a Comment