SPORTS: Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu anatarajiwa kuwa nje kwa miezi mitatu kutokana na maumivu ya goti la mguu wake kushoto. Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Eskilstuna nchini Sweden, Ulimwengu amesema kwamba amepokea taarifa za kusikitisha kutoka kwa Daktari wa timu yao.
"Juzi nilikwenda kupimwa na jana nikakutana na Daktari, maana nilivyoshitua goti kwenye mechi ya kirafiki nilianza maozezi ila bado ukawa unaendelea kuuma, hivyo jana ndiyo nimepewa hizi taarifa,"amesema Ulimwengu.Thomas Ulimwengu atakuwa nje kwa miezi mitatu kutokana na maumivu ya goti la mguu wake kushoto
Amesema ameambiwa anatakiwa kuwa nje kwa miezi mitatu kutokana na maumivu ya goti, baada ya vipimo alivyofanyiwa juzi nchini humo kufuatia kuumia Machi 23, akicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Malmo FF.Hakika huu ni mwanzo mbaya kwa Ulimwengu aliyejiunga na Eskilstuna Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya AFC Eskilstuna ya Sweden, alikocheza hadi mwaka 2011 alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.Ulimwengu amehamia Ulaya baada ya kushinda mataji makubwa akiwa na Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.
No comments:
Post a Comment