Magoli ya Mbao yamefungwa na Sangija dakika ya 18 na Bernard aliyefunga goli dakika ya 33. Hadi dakika ya 80 Simba ilikuwa nyuma kwa magoli 2-0 matokeo ambayo kama yangebaki hivyo dakika 90 zinamalizika basi Wekundu wa Msimbazi wangekuwa kwenye nafasi finyu ya kutwaa taji la ligi kuu msimu huu.
Mabadiliko yaliyofanywa na benchi la ufundi la Simba kwa kumtoa Pastory Athanas na nafasi yake kuchuliwa na Said Ndemla, Blagnon na Mavugo wakaingia kuchukua nafasi za Liuzio na Hamad ndiyo yaliyo badili mchezo na kuipa Simba ushindi wa kwanza Kanda ya Ziwa msimu huu baada ya kuchapwa 2-1 na Kagera Sugar Jumapili iliyopita.
Magoli ya Simba yamefungwa dakika za lala salama ambapo goli lao la kwanza limefungwa dakika ya 82 na Frederick Blagnon. Uzembe wa golikipa wa Mbao Erick Ngwegwe ambaye aliuacha mpira udunde kisha akashindwa kuudaka kwa usahihi ulitua miguuni mwa Blagnon akafunga goli la pili dakika ya 90+1 na kufanya matokeo kuwa 2-2.
Wakati kila mmoja akiamini mchezo utamalizika kwa sare ya Mbao 2-2 Simba, Mzamiru Yassin akaifungia Simba goli la tatu dakika ya 90+7 kwa shuti kali baada ya beki wa Mbao kupiga kichwa mpira ambao ulitua kwa Mzamiru kisha kiungo huyo wa Simba kuachia mkwaju uliomshinda mlinda mlango wa Mbao.
Ushindi huo unaifanya Simba ifikishe pointi 58 ikiwa imecheza mechi 26 na kurejea kwenye nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi kwa pointi mbili zaidi ya Yanga wanaoshuka kwenye nafasi ya pili lakini wakiwa na faida ya mechi moja mkononi.
Swali ambalo mashabiki wengi wa Simba huenda wakawa hawajalipatia majibu ni kwanini Ibrahim Ajib, Laudit Mavugo, Said Ndemla na golikipa Daniel Agyei kuanzia nje wakati wanne hao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mechi za hivi karibuni?
No comments:
Post a Comment