SPORTS: uongozi wa Simba uliita waandishi wa habari kwa ajili ya kuzungumza nao na kuweka wazi msimamo wao kuhusu sakata la pointi tatu linalozihusu klabu mbili ambazo ni Simba pamoja na Kagera Sugar.
Uongozi wa Simba kupitia kwa afisa habari wao Haji Manara umesema, Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za wachezaji haikustahili kukaa kikao cha kupitia maamuzi yaliyotolewa na kamati ya saa 72 badala yake kamati ya saa 72 ndiyo yenye mamlaka ya kupitia uamuzi wake kama ilivyoombwa na klabu ya Kagera Sugar.
“Kikao ambacho hakina uhalali wa kufanya review kwa sababu sio kikao cha awali kilicho cha kamati ya saa 72 ambacho ndicho kilipaswa kufanya review kikaa kwa muda wa zaidi ya saa 10 kikiwahoji meneja, katibu na mchezaji aliyepewa kadi kitu ambacho hakijawahi kutokea popote kihistoria.”
“Kikao kile kilikuwa hakina haki ya kuzungumza wala kujadili, wanasema ile ni kamati ya sheria ina haki ya kuingilia kamati nyingine, jana nilimsikia Katibu Mkuu wa TFF Mwesigwa Selestine anasema wanafanya mwendelezo wa kikao cha kamati ya saa 72. Mwendelezo kivipi wakati barua ya Kagera Sugar imetaka review na sio mwendelezo?”
Manara pia akaonesha wasiwasi wake juu ya kucheleweshwa kwa maamuzi huku akihoji uhalali wa kuhojiwa kwa baadhi ya mashadi ambapo amesema, kuna baadhi ya mashahidi hawakustahili kutoa ushahidi wao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
“Musa Mgosi wakati anacheza Simba iliponyang’anywa pointi hakuitwa popote kuhojiwa, Azam iliponyang’anywa pointi kwa kumchezesha Erasto Nyoni aliyekuwa na kadi tatu za njano hakuitwa popote kwa ajili ya kuhojiwa. Hakuna mchezaji anayeitwa kuhojiwa kokote duniani, kinachoangaliwa ni ripoti ya mwamuzi, kwetu wameitwa hadi waamuzi wasaidizi lakini kama haitoshi ameitwa hadi fourth official ili ahojiwe.”
Manara akaituhumu TFF kuwa inapendelea katika kutoa baadhi ya maamuzi yake juu ya makosa ya wachezaji na vilabu kwa kuorodhesha matukio kadhaa ya kinidhamu na hatua zilizochukuliwa na TFF.
“Tumeshawahi kulalamika kuhusu Donald Ngoma kumpiga Hassan Kessy wakati yupo Simba, lakini kamati ya nidhamu ipo kimya miaka miwili sasa. Juma Nyoso alifungiwa kwa kumshika John Bocco sehemu zisizo stahili, kitendo alichofanya Tambwe kwa kumshika Juuko Murshid sehemu za siri na picha zikazagaa mitandaoni lakini hajafungiwa. Kitendo walichofanya wachezaji wa Yanga cha kumbeba mchezaji wa African Sport aliyeumia uwanjani na kumbwaga nje nani alizungumza? Lakini Banda alimpiga mchezaji wa Kagera Sugar hata wiki haikuisha akasimamishwa, japo Simba haitetei kitendo kilichofanywa na Banda.”
No comments:
Post a Comment